Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Mipango

HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI
27 Apr, 2024
HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), amewasilisha bajeti ya wizara yenye Vipaumbele 10 vitakavyotekelezwa mwaka 2024/25.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25 leo Bungeni jijini Dodoma, Prof. Mkumbo amesema kuwa bajeti hiyo imebeba malengo ya kuratibu mipango thabiti inayolenga kuleta maendeleo endelevu na jumuishi kwa wananchi; kuvutia uwekezaji wenye tija kwa Taifa; uboreshaji wa mazingira ya biashara; na uendeshaji wenye tija wa mashirika na taasisi za umma. 

"Katika kufikia lengo hili, programu, miradi na kazi zitakazotekelezwa na Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji umezingatia vipaumbele kumi" Alisema Prof. Mkumbo.

Akitaja vipaumbele hivyo, Prof. Mkumbo amesema pamoja na kukamilisha maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2050 na kukamilisha uandaaji wa sera mpya ya uwekezaji na mkakati wake wa utekelezaji.

Vipaumbele vingine ni, kukamilisha uunganishaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Maeneo ya Uzalishaji wa Mauzo ya Nje (EPZA) na kuanzisha Taasisi mpya ya kusimamia masuala ya Uwekezaji wa sekta Binafsi. 

Prof. Mkumbo ameongeza kuwa Ofisi yake, itakamilisha mwongozo wa ujenzi na uendeshaji wa kongani za viwanda nchini na Kufanya tathmini kuhusu uanzishwaji na uendeshaji wa maeneo maalum ya kiuchumi (special economic zones) nchini.

Aidha, Kufanya mapitio ya Sheria zinazohusu masuala ya madini, ardhi, kilimo, utalii na biashara kwa ajili ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini; na kukamilisha kutungwa kwa Sheria ya Uwekezaji wa Umma na Kanuni zake ni maeneo mengine yatakayotiliwa mkazo.

"Kuanza utekelezaji wa mradi wa kielelezo wa Ukanda Maalum wa Kiuchumi Bagamoyo (Bagamoyo Special Economic Zone - BSEZ) kwa kuzingatia Mpango Kabambe wa mwaka 2024" alisema.

Vipaumbele vingine ni Kuanzisha mashindano ya jinsi Sekretariati za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinavyovutia uwekezaji na kuweka mazingira bora ya uwekezaji na biashara; na Kuhuisha Mpango wa Maboresho wa Mazingira ya Biashara na Uwekezaji utakaoainisha changamoto mpya za Uwekezaji na Biashara nchini, na namna ya kuzishughulikia changamoto hizo.

Hii ni bajeti ya kwanza ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kuwasilishwa bungeni tangu kuanzishwa kwake.