Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Taifa ya Mipango

NPC Yaendelea Kushirikiana na UNDP katika Urasimishaji wa Ufadhili Bunifu na Mageuzi ya Kimuundo kwa Utekelezaji wa DIRA 2050
26 Aug, 2025
NPC Yaendelea Kushirikiana na UNDP katika Urasimishaji wa Ufadhili Bunifu na Mageuzi ya Kimuundo kwa Utekelezaji wa DIRA 2050

Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango (NPC), Dkt. Fred Msemwa, amesema kuwa matumizi ya mifumo bunifu ya ugharamiaji—ikiwemo mitaji ya kimkakati, mifumo imara ya mazingira wezeshi kwa kampuni changa, pamoja na ushiriki mpana wa sekta binafsi—ni muhimu katika kuchochea mageuzi jumuishi ya kiuchumi nchini Tanzania.

Dkt. Msemwa alitoa kauli hiyo leo (11.12.2025) jijini Dodoma wakati wa kikao na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Shigeki Komatsubara, ambaye alitembelea ofisi za Tume kwa mazungumzo ya kujadili maeneo ya uwezekano wa ushirikiano kati ya NPC na UNDP.

Alibainisha kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mageuzi makubwa ya kimkakati na ya kimuundo ili kuondoa vikwazo katika utekelezaji wa Dira 2050, ambayo inalenga kuielekeza nchi kufikia uchumi wa thamani ya dola za kimarekani  trilioni 1 ifikapo mwaka 2050.

“Ushiriki hai wa sekta binafsi, pamoja na mageuzi shirikishi ya sera na miundo, ni muhimu katika kujenga uchumi jumuishi kwa Watanzania wote,” alisema Dkt. Msemwa.

Aidha, Dkt. Msemwa aliongeza kuwa sekta kadhaa za kipaumbele—ikiwemo kilimo, utalii, michezo, usafirishaji na usambazaji , madini, na nishati—zimechaguliwa kimkakati ili kuharakisha mageuzi ya uchumi na kuzalisha ajira nyingi, hususan kwa vijana.

Kwa upande wake, Bw. Komatsubara alisisitiza umuhimu wa kutumia mtazamo jumuishi katika mabadiliko ya kimuundo na kudumisha mwelekeo kwenye malengo ya muda mrefu ya maendeleo.

“NPC ina nafasi muhimu sana. Nikiwa natoka Japan, nimeona jinsi mabadiliko makubwa yanavyohitajika katika kujenga uchumi wenye usawa na jumuishi kupitia utekelezaji wa dira ya taifa,” alisema Bw. Komatsubara, akiongeza: “Furaha na ustawi ni muhimu kwa kila mwananchi.”

Tume ya Taifa ya Mipango ilianzishwa chini ya Sheria ya Tume ya Mipango, Sura ya 127, ikiwa na majukumu mbalimbali yakiwemo kuratibu usimamizi wa uchumi, mipango ya maendeleo na utekelezaji wa mipango iliyoidhinishwa ya maendeleo.

Tume ya Taifa ya Mipango inafanya kazi chini ya Kamisheni inayoongozwa na Rais, ambayo ndiyo chombo cha juu kabisa cha ushauri kwa Serikali kuhusu masuala ya usimamizi wa uchumi na mipango ya maendeleo.

Pamoja na majukumu mengine, Tume ya Taifa ya Mipango ina wajibu wa kuandaa mipango ya maendeleo ya taifa ya muda mrefu, wa kati na  mfupi. Zaidi ya hayo, Tume ina jukumu la kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo, ikijumuisha miradi kielelezo na ya kimkakati, kwa lengo la kuendeleza maendeleo ya taifa. Vilevile, Tume inawajibika kuandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa, ambayo hutumika kama mwongozo mkuu wa upangaji wa maendeleo ya nchi.