Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Mipango

Wajibu na Majukumu

Wajibu na Majukumu ya Tume ya Mipango ni kama ifuatavyo:

  1. Kutathmini hali ya rasilimali za taifa na kuishauri serikali kuhusu matumizi bora ya rasilimali hizo;
  2. Kuandaa dira ya maendeleo ya taifa, mpango wa maendeleo wa muda mrefu, mpango wa maendeleo wa muda wa kati na mpango wa maendeleo wa muda mfupi, na kusimamia utekelezaji wake;
  3. Kupendekeza maeneo ya miradi endelevu ya kielelezo na mikakati ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuzingatia dira na mikakati ya maendeleo ya taifa;
  4. Kufanya tathmini na uchambuzi wa mara kwa mara wa viashiria muhimu vya uchumi ambavyo vinajumuisha urari wa malipo, mtiririko wa fedha na bei, deni la taifa na kuishauri serikali ipasavyo;
  5. Kutathmini sera mbalimbali zilizopo kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wake kwa kuzingatia mipango ya maendeleo ya taifa na kupendekeza sera mpya pale inapoonekana inafaa kwa maslahi ya taifa;
  6. Kufuatilia utekelezaji wa maeneo muhimu ya vipaumbele vya taifa kwa sekta mbalimbali za uchumi na kuhakikisha kuwa hatua stahiki zinachukuliwa ili kutatua changamoto zozote za uendeshaji zitakazobainika katika sekta hizo;
  7. Kutoa mwongozo kuhusu ushirikiano wa kiuchumi kati ya jamhuri ya muungano na nchi nyingine na mashirika ya kimataifa;
  8. Kuhakikisha mipango ya sekta inafungamanishwa na mipango ya taifa ili kuwa na matumizi yenye tija ya rasilimali za nchi;
  9. Kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango ya kitaifa na miradi ya kielelezo na kuchukua hatua zinazohitajika ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi;
  10. Kuishauri serikali kuhusu mabadiliko yoyote katika mpango wa maendeleo wa taifa ulioidhinishwa;
  11. Kufuatilia utekelezaji wa maamuzi ya baraza la mawaziri kuhusu masuala ya mipango ya maendeleo na usimamizi wa uchumi;
  12. Kushauri kuhusu mikakati ya kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu nchini;
  13. Kukuza mbinu za ubunifu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo;
  14. Kutambua na kufanya utafiti kuhusu suala lolote ambalo tume inaona ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa;
  15. Kusimamia na kutoa mwongozo katika uandaaji wa mipango mkakati iliyoandaliwa na wizara, idara zinazojitegemea, wakala za serikali, sekretarieti za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na taasisi nyingine za umma;
  16. Kuratibu na kuendeleza kada za mipango, uchumi na takwimu na taaluma nyingine zinazofanana na hizo;
  17. Kuratibu makongamano ya wadau mbalimbali kwa ajili ya kujadili masuala ya mipango ya maendeleo;
  18. Kubainisha rasilimali za nchi kwa matumizi endelevu kwa maendeleo ya taifa;
  19. Kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi katika upangaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo; na
  20. Kutekeleza majukumu mengine yanayohusiana na mipango ya maendeleo kadri rais atakavyoelekeza.