Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Mipango

NAIBU WAZIRI MIPANGO NA UWEKEZAJI AHIMIZA MAJADILIANO YENYE TIJA, KUPATIKANA DIRA 2050
11 Jan, 2025
NAIBU WAZIRI MIPANGO NA UWEKEZAJI AHIMIZA MAJADILIANO YENYE TIJA, KUPATIKANA DIRA 2050

Akifungua Mkutano wa Asasi za Kiraia nchini Tanzania, wanaokutana kwaajili ya mapitio ya Rasimu ya kwanza ya dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo (Mb,)amekumbusha umuhimu wa majadiliano ya pamoja badala ya ukosoaji, ili kujenga uelewa wa pamoja utakaofanikisha upatikanaji wa Dira 2050 itakayotokana na Maoni ya wananchi na wadau mbalimbali kama ilivyokuwa dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.

Mhe. Nyongo ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar Es salaam, akisema wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma za maendeleo ya Jamii alikutana mara kwa mara na Asasi hizo za kiraia, akisema usipoelewa dhamira yao ya kukumbusha baadhi ya mambo, huenda ukafikiri kuwa wanaikosoa serikali kila wakati jambo ambalo sio la kweli.

Ameeleza kuwa kama Serikali wamejiandaa vya kutosha kusikiliza kila maoni ya Wadau na Wananchi, akisema jambo hilo ni muhimu zaidi ili kuhakikisha kuwa Dira 2050 inakuwa halisi na inayotokana na maoni ya wananchi.