Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Mipango

JINSIA NA KIPAUMBELE KATIKA UKUAJI WA IDADI YA WATU NA MAENDELEO
30 Apr, 2024
JINSIA NA KIPAUMBELE KATIKA UKUAJI WA IDADI YA WATU NA MAENDELEO

Katibu Mtendaji Bw. Lawrence Mafuru ameongoza kikao kazi cha usambazaji wa taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa Azimio la Addis Ababa kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo, akishirikiana na Bi. Rahma Mahfoudh, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, na Bw. Mark Bryan Schreiner, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Idadi ya Watu Tanzania. Kikao hicho kilijumuisha makatibu wakuu kutoka serikalini, wakurugenzi wa idara za sera na mipango, pamoja na maafisa waandamizi kutoka wizara mbalimbali.

Bw. Mafuru alisisitiza umuhimu wa kuzingatia masuala ya idadi ya watu katika upangaji wa maendeleo, akisema kwamba maendeleo ni kwa ajili ya watu na ili maendeleo yatokee, yanahitaji watu. Alieleza pia kwamba imebaki miaka sita tu kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hivyo ni muhimu kutafakari juu ya maendeleo ya Azimio la Addis Ababa la mwaka 2014.

Washiriki wa kikao walipata fursa ya kutoa maoni na kupata ufafanuzi katika maswali mbalimbali, ili kuwa na uelewa sahihi wa masuala yaliyowasilishwa na kujadiliwa. Bi. Rahma Mahfoudh alieleza kuwa taarifa hiyo ni kama ramani inayoonyesha hatua na juhudi zilizochukuliwa katika kujenga mustakabali bora wa maisha ya watanzania, na kusisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja na ushirikiano ili kuwa na matokeo makubwa zaidi na yenye tija.