Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Mipango

KAMATI YA VIONGOZI WA DINI YAHAKIKI RASIMU YA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050.
14 Jan, 2025
KAMATI YA VIONGOZI WA DINI YAHAKIKI RASIMU YA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ameweka bayana mwelekeo wa Taifa kupitia Dira mpya ya Maendeleo 2050, akisisitiza umuhimu wa kujenga taifa jumuishi lenye ustawi, haki, na linalojitegemea.

Akizungumza Jumatatu, Januari 13, 2025, katika Mkutano wa Kamati ya Dini Mbalimbali Kuhakiki Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa TEC, Kurasini, Dar es Salaam, Prof. Kitila ameelezea mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya miaka 25 iliyopita.

“Tunahitimisha rasmi zoezi la kukusanya maoni ya uhakiki ya Rasimu ya Dira 2050. Tunakutana na taasisi za dini kwa sababu mnakusanya jamii kubwa ya Watanzania, na maoni yenu tunaamini yanaakisi maoni ya wengi,” amesema Prof. Kitila.

Prof. Kitila amebainisha kuwa tangu mwaka 2000, Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye sekta mbalimbali ikiwamo elimu ambapo idadi ya wanafunzi wa shule za msingi wanaoendelea na sekondari iliongezeka kutoka chini ya 20% mwaka 2000 hadi 78% mwaka 2024, huku lengo likiwa ni kufikia 90% mwaka 2025.

Aidha ameeleza kuwa sekta kama afya, umeme, na maji zimepiga hatua kubwa, na huduma zimeboreshwa kwa wananchi wengi Zaidi, na kwamba uchumi wa taifa umekua kwa wastani wa 6.7% katika miaka 20 iliyopita, ingawa lengo lilikuwa ukuaji wa 8-10%.

Akizungumzia rasimu ya Dira mpya, Prof. Kitila amesema kuwa ifikapo mwaka 2050, Tanzania inalenga kuwa na uchumi wa kati wa hadhi ya juu, wenye pato la taifa zaidi ya dola bilioni 500, kuongeza pato la mtu mmoja hadi kufikia zaidi ya dola 4,700 kwa mwaka, na kujenga uchumi jumuishi unaopunguza umasikini na kuongeza ustawi wa wananchi wote.

“Kama taifa, tunapendekeza njozi yetu kuu kuwa ni kujenga taifa jumuishi lenye ustawi, haki, na linalojitegemea,” amesisitiza Prof. Kitila.

Prof. Kitila ametoa wito kwa viongozi wa dini kushirikiana na serikali katika kutekeleza maono haya, akisisitiza umuhimu wa mshikamano wa kitaifa katika kufanikisha dira hiyo”