Kilele cha Siku ya Idadi ya Watu Duniani Chafanyika Kitaifa Mkoani Geita
Geita, Tanzania – Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani kimefanyika leo tarehe 11 Julai 2024 katika Kituo cha Maonyesho cha Kibiashara (EPZA) kilichopo Bombambili, Mkoani Geita. Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo, alihudhuria kama mgeni rasmi.
Maadhimisho haya, ambayo hufanyika kila mwaka duniani kote, yalizinduliwa rasmi tarehe 11 Julai 1989 baada ya idadi ya watu duniani kufikia bilioni tano. Tanzania imekuwa ikiadhimisha siku hii tangu ilipojiunga na Umoja wa Mataifa, ambapo Serikali kupitia Tume ya Mipango inashirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA), pamoja na mashirika na asasi za kiraia.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Nyongo alisisitiza umuhimu wa takwimu sahihi katika uandaaji wa mipango na mikakati ya maendeleo. “Ni wazi kuwa Mkoa wetu pamoja na mikoa mingine bado inakabiliwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu lisiolendana na kasi ya ukuaji wa uchumi na ubora wa watu husika ,Maadhimisho haya yalete chachu ya matumizi ya takwimu katika uandaaji wa mipango na mikakati ya maendeleo ili kuwafikia watu walio wengi na kuwa na maendeleo yenye usawa”amesema Mhe. Nyongo."
Lengo kuu la maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani ni kuhakikisha kuwa kuna mipango bora inayowiana na ongezeko la idadi ya watu, ili kufikia maendeleo endelevu.