RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN KUTOA UJUMBE MAALUM KATIKA KUADHIMISHA MIAKA 62 YA UHURU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kutoa ujumbe maalum katika kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania katika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Kitaifa wa Dira ya Maendeleo ya Taifa utakaofanyika Disemba 9, 2023 jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema hayo leo Disemba 1, 2023 jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano huo.
"Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atafungua Mkutano wa Kwanza wa Kitaifa wa Dira ya Maendeleo ya Taifa utakaofanyika siku ya Jumamosi, tarehe 9 Disemba 2023 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam," amesema Prof. Mkumbo.
Amesema, kwa kuwa mkutano huo unafanyika siku ya Uhuru, hivyo Mhe. Rais anatarajia kutumia siku hii kutoa ujumbe maalum katika kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Prof. Kitila amesema lengo kuu la mkutano huo ni kuzindua, kupokea na kujadili taarifa ya kitafiti ya tathimini ya Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
"Dira hii ilianza kutekelezwa mwaka 2000 na itafika mwisho wake mwaka 2025. Pamoja na mafanikio mengine, taarifa ya tathimini inaonesha kuwa pato la Mtanzania (GDP per capital income) limeongezeka kutoka dola za kimarekeni 399.5 (TZS 322,597) mwaka 2000 hadi kufikia dola za kimarekani 1,200 (TZS 2,880,000) mwaka 2022," amesema Prof. Mkumbo.
Amesema Tanzania imefikia asilimia 124 ya kujitosheleza kwa chakula ikilinganishwa na lengo la kufikia asilimia 140 ifikapo mwaka 2025. Hatua hii imewezesha Tanzania kukabiliana na njaa kwa mikoa na wilaya zote nchini. Vilevile mtandao wa barabara za lami na zege (paved roads) katika mikoa umeongezeka kutoka KM 4,179 mwaka 2000 hadi kufikia KM 11,966.38 mwaka 2023.
Aidha, mkutano huo utahudhuriwa na wadau 971 wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa taasisi za dini, viongozi wa taasisi mbalimbali za sekta binafsi, viongozi wa makundi mbalimbali ya kijamii, yakiwemo wazee watu wenye ulemavu, wakulima, wafugaji, wavuvi, na wachimbaji madini, jumuiya ya kimataifa, wasomi, Waandishi wa Habari.