SERIKALI YAWEKA MSUKUMO WA KUIMARISHA SEKTA YA MIPANGO NCHINI
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msukumo wa kipekee wa kuimarisha Kada ya Wanamipango nchini ili Taifa liweze kufanikisha mipango yake inayotekelezeka kwa maendeleo ya watu wake wa kizazi cha sasa na kijacho.
Akizungumza leo jijini Arusha wakati akifungua Kongamano la Wanamipango la mwaka 2023, Mhe. Naibu Waziri Mkuu amesema "Mhe. Rais ameweka msukumo mkubwa hata wa kuanzisha Tume ya Mipango ambayo ina kazi hii tunayoiona leo, katika hatua nyingine Serikali imeanzisha Kitengo cha Tathmini na Ufuatiliaji katika Wizara na Taasisi zote za Serikali kwa lengo la kuimarisha jukumu la ufuatiliaji wa mipango yetu, pia kuongeza uwajibikaji na uwazi katika kutekeleza jukumu la ufuatiliaji wa tathmini katika Wizara na Taasisi zetu".
Ameongeza kuwa, lengo la kuanzisha kwa Vitengo hivyo ni moja ya jitihada za Mhe. Rais ambapo amekuwa na maono ya muda mrefu ili vitengo hivyo viweze kuongeza tija katika Serikali
Aidha, ametoa rai kwa Wanamipango nchini kuwa mstari wa mbele kuhakikisha mipango inayopangwa iwe dira ya kuifanya Serikali kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia mipango na sio fikra za mtu mmoja mmoja.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo awali wakati akimkaribisha mgeni rasmi amesema kuwa Wanamipango wanatakiwa kutokuwa na huruma katika kuchagua vipaumbele vya mipango na katika utekelezaji wake.
"Tukishapanga lazima tutekeleze na lazima kuwe na athari za kutotekeleza kwa wakati na pia kutokuwa na huruma katika kuendeleza, na watu wa kuhakikisha kunakuwa na uendelezaji ni hawa Wakurugenzi wa Sera na Mipango", ameeleza Prof. Kitila.
Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida amesema kuwa Kongamano hilo la Wanamipango ni la kwanza tangu Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipounda Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na kutungwa kwa Sheria ya Tume ya Mipango ya mwaka 2023.
Ameongeza kuwa Kongamano hilo linalokutanisha Wanamipango kutoka katika nyanja mbalimbali linafanyika wakati ambao uwepo wa Tume ya Mipango utawezesha namna ya kuunganisha mawazo katika utekelezaji wa shughuli za upangaji wa pamoja hasa ikizingatia kuwa kauli mbiu yake ni 'Fikra za Pamoja na Utekelezaji Ulioratibiwa kwa Ukuaji wa Uchumi Jumuishi'.
Dkt. Kida amesema "Wataalamu tutakuwepo hapa wiki nzima tukijadili mada na mijadala mbalimbali muhimu itakayolenga kupata mawazo yatakayosaidia maendeleo ya nchi yetu ambayo ni jumuishi kwa watu wote".