TUME YA TAIFA YA MIPANGO YAFANYA KIKAO KAZI CHA MAANDALIZI YA AJENDA YA TAFITI ZA KIMKAKATI.
Dodoma, Tanzania – Naibu Katibu Mtendaji anayeshughulikia Biashara na Ubunifu, Dkt. Lorah Madete, leo Januari 14, 2025, amefungua kikao kazi maalum cha maandalizi ya ajenda ya tafiti za kimkakati. Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma kikihusisha wadau mbalimbali, wakiwemo Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa COSTECH, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Wakurugenzi Wasaidizi wa Sera, Tafiti na Ubunifu, pamoja na wajumbe wengine kutoka kada husika.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Dkt. Madete amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu katika kufanikisha tafiti zitakazosaidia katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP III) na maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Mwaka 2023, Serikali ilirejesha Tume ya Taifa ya Mipango kwa lengo la kusimamia uchumi wa taifa na kuhakikisha mipango ya maendeleo inaandaliwa na kutekelezwa kwa namna itakayohakikisha ukuaji endelevu wa uchumi. Mafanikio hayawezi kufikiwa bila ushirikiano wa wadau pamoja na upatikanaji wa taarifa sahihi kwa ajili ya maamuzi na upangaji wa mipango yenye tija,” alisema.
Dkt. Madete amebainisha kuwa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) unasisitiza umuhimu wa tafiti huru na bunifu katika kujenga uchumi wa viwanda na ushindani. Alinukuu nyaraka za Mpango huo zinazosema: “Matokeo ya tafiti huru yatasaidia kuimarisha utekelezaji wa Mpango na hatua za kimkakati.”
Katika maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, tafiti na teknolojia zimewekwa kuwa nguzo muhimu. Rasimu ya Dira hiyo imeeleza kuwa mabadiliko ya kiteknolojia yanayoshuhudiwa kwa kasi kubwa yanaweza kuwa chachu ya maendeleo, lakini pia yameambatana na changamoto, hususan katika suala la ajira kwa vijana.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, Tume ya Taifa ya Mipango imependekeza ajenda ya utafiti ya kimkakati inayojulikana kama “Ajira katika Kipindi cha Mabadiliko ya Kasi ya Kiteknolojia.” Ajenda hii inalenga kuoanisha maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira kwa vijana.
Dkt. Madete amewataka washiriki wa kikao hicho kutumia muda wa siku mbili za kikao kazi kujadili na kuchambua kwa kina namna bora ya kuendeleza tafiti na ubunifu zitakazosaidia kutatua changamoto za sasa na zijazo.
“Tunashuhudia kasi kubwa ya maendeleo ya kiteknolojia ambayo hayakwepeki. Ni muhimu tuangalie namna ya kuzitumia fursa hizi kwa manufaa ya taifa letu huku tukitafuta mbinu za kukabiliana na changamoto zinazoambatana nazo. Tafiti zenye tija zitatoa mwongozo bora wa sera na mipango ya maendeleo,” alisisitiza.
Kikao kinatarajiwa kufanikisha mapendekezo ya ajenda ya utafiti ya kimkakati itakayoongoza maandalizi ya mipango na mikakati ya maendeleo ya Taifa kuelekea mwaka 2050. Wataalamu mbalimbali wanatarajiwa kutoa mawasilisho kuhusu ukuaji wa teknolojia, ajira za baadaye, na mchango wa vijana katika maendeleo ya taifa.